Shilole Ahusika Kwenye ‘Mjengo’ wa Man Fongo
Mkali wa muziki wa singeli Bongo, Man Fong amemtaja msanii mwenzake wa bongo fleva na bongo movie, Shilole a.k.a Shishi Trump kuhusika katika ujenzi wa nyumba yake ambayo anataraji kuijenga wakati wowote kutoka sasa.
Man Fongo aliyekuwa katika mahojiano kwenye kipindi cha Ujenzi cha EATV, amesema mtu pekee aliyemuhamasisha kujenga nyumba ni Shilole, na hiyo ni baada ya siku moja kutembeea nyumbani kwa Shilole na kukuta vitu ambavyo yeye aliona ni vya ajabu na kujikuta anavipenda na kutamani kuwa navyo katika nyumba yake.
Alisema jambo la kwanza alilofanya kukusanya fedha na kununu kiwanja ambacho kiko tayari na amekinunua maeneo ya Kimara Bonyokwa na muda wowote ataanza kuporomosha mjengo wake.
Amesema hawezi kumsahau Shilole kwa kumpa hasira za kuweka mjengo huo, ambao amesema ataujenga taratibu kwa kadri atakavyokuwa anapata pesa na anatamani uwe na vitu vyote vizuri kama ambavyo huwa anaviona kwa washkaji zake hasa Shilole, licha ya kuwa yeye ni mtoto wa uswahilini.
“Sina nyumba, lakini nina kiwanja Kimara Bonyokwa na Shilole ndiye aliyenipa hasira ya kumiliki mjengo wangu, mimi ni mtu wa uswazi lakini kuna vitu ningependa kuviweka kwenye mjengo wangu, natamani kuwa na vitu vizuri, kama ninavyoona kwa wenzangu….. kwa mfano pale kwa Shishi nimeona amechora chora hivi kwa pembeni, halafu juu kuna madude hivi mimi huwa naita ceiling board, nyie sijui mnaitaje (Gypsum) eheee” Amesema Man Fongo.
Amewashauri vijana hususani wasanii wenye uwezo na kipato kujenga nyumba zao, kwani ni muhimu na si lazima kujenga haraka bali kwa utaratibu kadri watakavyokuwa wakipata pesa.
“Kama mimi ndo nimeanza kupata kipato changu kidogo, nimeanza kununua kiwanja… kujenga hakuhitaji papara, kama leo ukishindwa, zamu yako itakuja kesho” Alimalizia Man Fongo
eatv.tv