Shilole; Kilichokupata Feri ni Sawa Tu, Kwa Nini Ulalamike?
ZUWENA Mohammed ndilo jina alilopewa na wazazi wake alipozaliwa nyumbani kwao Igunga, mji mdogo, lakini maarufu mkoani Tabora. Lakini katika harakati za maisha, amejikuta akipata umaarufu mkubwa nchi nzima na jirani, kwa jina lake la kisanii la Shilole.
Wengine wanamuita Shishi Baby. Huyu anathibitisha kuwa mwanamke akiamua, inawezekana. Kwa sababu historia yake inaonesha kuwa ni mpambanaji, akitokea kudhalilishwa kimapenzi akiwa na umri mdogo, hadi kuja kuwa staa mkubwa.
Katika muziki, anafanya vizuri sana, kwani kila kukicha, anaonesha kuendelea, akifanya aina ya muziki ambao awali ulikuwa Mduara, lakini kwa sasa ameuongeza vionjo vinavyomfanya kuwa kivutio cha aina yake stejini.
Ana kazi nyingi nzuri, tangu alipoanza na wimbo wake wa Lawama, zikiwemo Dume Dada, Paka la Bar, Chuna Buzi, Namchuka, Malele, Nyang’angany’a na sasa kibao kipya alichomshirikisha Barnaba, Say My Name.
Hata hivyo, kama ilivyo kwa binadamu wote, nje ya sanaa, ana maisha binafsi yanayoendana na matukio ambayo mengi yanachagizwa na ustaa wake. Kwa mfano juzikati, akiwa na washkaji ndani ya pantoni kuelekea Kigamboni.
Akiwa ndani ya gari na kidogo akionekana kuchangamka, alikataa kushuka garini kama utaratibu ulivyo. Gari halitakiwi kupakiwa kwenye pantoni likiwa na abiria, anatakiwa dereva tu, ili aweze kulidhibiti endapo kutatokea dharura yoyote.
Shishi Baby alikataa katakata kushuka, akiwaambia walinzi kuwa yeye ni staa mkubwa, hivyo aachwe avuke akiwa ‘amejilalia’ zake garini, jambo ambalo halikukubaliwa, hivyo kuwafanya walinzi hao kumshusha kwa nguvu na ‘kumpumzisha’ kwa muda ili kiburudisho alichopata kipunguze makali.
Hili ndilo tatizo moja kubwa sana kwa hawa mastaa wetu, hasa hawa wa dotcom. Wanaamini kujulikana kwao ndiyo leseni ya kufanya wanavyotaka, bila kujali kuwa kuna sheria na taratibu ambazo lazima zifuatwe, bila kujali ‘taito’ yako, iwe msanii, mwanasiasa, mwanasheria au yeyote yule.
Na ubaya zaidi, hawafahamu kuwa wao ndiyo wanastahili kuwa namba moja katika kuzifuata na kuzitii sheria na taratibu hizo, ili wawe mifano kwa wengine, hasa mashabiki wao.
Inashangaza kuwa hawafahamu kwamba kuna watu ukiwatajia Shilole wala hata hawaelewi unasema nini. Siyo kila mtu anafuatilia muziki, filamu au chochote unachokifanya. Sasa unapoingia kwenye kazi ya mtu na kusema eti; ‘kwani hunijui mimi?’ unampa majaribu tu ya bure. Kwani wewe nani katika nchi hii?
Unaweza kufika ofisi ya umma na kujitambulisha, ukitegemea kila mtu anakufahamu, hapana. Kuna wengine hawafuatilii kabisa Bongo Fleva, hawajui hata filamu za Kibongo zikoje, sasa wakisema hawakujui usifikiri wanatania na hata kama wanakujua, ndiyo uvunje sheria?
Nimshauri tu dada yangu Shilole, katika kufuata sheria na taratibu, anapaswa kuwa mstari wa mbele ili wanaomshabikia nao watambue kuwa wanapaswa kuzingatia, vinginevyo kama unataka kuutumia ustaa, basi ni kwenye viwanja vya burudani ambako wanaofika ni wale wanaokufahamu.
Chanzo:GPL