SHILOLE msimchukulie poa kabisa. Alichopanga kufanya kama kikikaa sawa, itakuwa gumzo kwelikweli hapa jijini.
Msanii huyo wa muziki wa Bongo Flava na mwigizaji wa Bongo Muvi amewaambia mashabiki na marafiki zake kwamba, wasiwe na haraka watulie kwanza kwani anaamini ndoa yake ambayo amedai iko njiani, itaacha historia.
Amesema kuwa harusi yake itakuwa ya maana na ya aina yake miongoni mwa wasanii wote wa Bongo.
“Watu wanazungumza sana kuhusu mimi kuolewa, lakini wasubiri wasiwe na haraka, ndoa inakuja punde na itakuwa bonge la harusi na kuacha historia Bongo nzima haijatokea kwani, ninajipanga si mchezo,” alisema Shilole, ambaye amekuwa kivutio kutokana na mbwembwe zake jukwaani na kwenye video zake na nyingine mbalimbali anazoshirikishwa.
Shilole siku za nyuma alikuwa na uhusiano na Nuhu Mziwanda, ambaye kwa sasa ameoa na kuna wakati ulizuka ubuyu kwamba etiii… wawili hawa bado wana uhusiano wa chini chini, lakini Shilole akasema wala sio kweli wakikutana ni ishu za kikazi zaidi.
Nuhu alioana na Nawal lakini waliachana na hivyo mashabiki wengi kudhani labda Nuhu na Shilole wamerudiana, jambo ambalo sio kweli.
Hata hivyo baada ya kusikia stori hizo, Shilole wala hakuonyesha kufurahia na kudai ni kitu cha kawaida wanandoa kuachana.
Kumekuwa na ishu za kutambiana kweli kweli miongoni mwa wasanii hasa wa Bongo Movie pindi wanapoolewa ama kuoa wakitaka kufunika sherehe zote zilizowahi kutokea hapo nyuma.
Kwa sasa Shilole anamiliki mgahawa wake unaomwingizia pesa nje ya muziki.
Mwanaspoti
Comments
comments