-->

SHILOLE : Macho ya Uchebe, Tabasamu Lake Miye Hoi

NAJUA unamjua ila Mpaka Home inakujuza zaidi. Siyo mwingine ni staa wa Bongofleva, Shilole maarufu kama Shishi Baby ambaye wazazi wake walimpa jina la Zuwena Mohammed.

Shishi ametamba na nyimbo kadhaa katika Bongofleva ingawaje umaarufu wake ulianzia kwenye filamu. Hivi karibuni, alifunga pingu za maisha na Ashraff Uchebe, watu wengi hawajui staa huyu anaishi vipi katika maisha yake ya ndoa.

Mpaka Home ilitinga Kinondoni Biafra jijini Dar es Salaam katika mgahawa wake ili kupiga naye stori kuhusu maisha mapya aliyoingia, ikiamini jamii inayomzunguka haifahamu undani wake.

ANAKUBALIKA UKWENI

Pamoja na kuwa na matukio mengi wakati akiwa anaibuka katika muziki kwa kuwa na wanaume tofauti, ilikuwa vigumu kumpata mwanaume atakayemfanya akukubalike ukweni, lakini hali imekuwa ndivyo sivyo. Shishi anakubalika ukweni kwake ile mbaya.

“Nashukuru Mungu wakwe zangu ni wacha Mungu na wananielewa na mimi niwaelewa vilevile, hawapendi kusikiliza maneno ya watu, wanatambua muda wa kazi ni upi na muda wa nyumbani upi, hivyo tunaishi Kizungu,” anafunguka. Shishi anaongeza mbali na wakwe zake kushika dini hata mume wake naye amebarikiwa katika hilo. Ni swala tano na hapendi kusikiliza mambo ya pembeni.

SHISHI FOOD ILIANZIA HOME

Hakuna asiyejua kama Shishi ni Maman’tilie, lakini alianzaje biashara yake hadi kumiliki mgahawa?

“Nilianzia kuuza chakula nyumbani kwangu kwa kuwapelekea baadhi ya watu majumbani kwao, lakini baadaye kila kukicha nikaona idadi inaongezeka, nikaona bora nitafute sehemu ambayo nitawapokea watu wengi, ndio nikapata hapa,” anasema.

Shilole aliongeza, katika biashara hiyo aliaanza na mtaji wa Sh 240, 000 tu, lakini kupitia kiasi hicho akajikuta akipata 500,000 kwa siku na ndipo maisha yakawa yameanza kubadilika polepole.

Pia, nyota huyo aliyezaliwa Desemba 20, 1987, alisema ana mpango wa kufungua Shishi Food katika mikoa ya Tabora hususan nyumbani kwao Igunga, Mwanza na Arusha.

AJIPANGA KWA LOUNGE

Shishi anayetamba na wimbo wa Kigori ni mwanamke mpambanaji ile mbaya, kwani baada ya kufanikisha kuwa na Shishi Food, yuko mbioni kukamilisha Lounge yake hivi karibuni.

“Namshukuru Mungu baada ya mapambano yangu, hivi karibuni natarajia kufungua Lounge yangu naamini watu watakuja na wataburudika kwa sababu chakula na vinywaji vyote vitakuwa vikipatikana hapa hapa.”

AZIKIMBIA FILAMU

Pamoja na kuanza kupata umaarufu wake kupitia filamu lakini Shishi hataki kabisa kusikia kuhusu filamu tena.

“Nimegeukia muziki kwa sababu unalipa, ukifanya wimbo wako mmoja mkali na ukapata shoo za kutosha utakuwa umeshafanikiwa, unakupa pesa nyingi, filamu mpaka upate pesa ya kulingana na muziki ni shida kidogo,” anafichua.

Pia, anaongeza filamu bado haijawabadilisha chochote na kuwafanya kufika mbali au kupiga pesa, badala yake wasanii wengi wameishia kukaa sehemu ileile bila kusogea mbele.

ATULIZWA NA UCHEBE

Mara nyingi Shishi anapenda kuwa muwazi katika mambo yake. Staa huyo anakiri siku za nyuma alikuwa hajatulia, akifanya vitu visivyoeleweka kutokana na kukosa mtu sahihi wa kumuongoza katika maisha yake.

“Unajua watu wengi niliokuwa nao awali walikuwa wanataka niendelee kujichetua. Sikuwa na mtu sahihi wa kuniongoza, lakini nikampata Uchebe ambaye ananikosoa na kunirudisha katika mstari, ndio maana hivi sasa nimebadilika tofauti na zamani.”

Huwezi kuamini hili lakini Shishi anatoa la moyoni kwa kukiri kuwa Uchebe ni mwanaume wa ndoto zake kwa sababu alikuwa akimhitaji mtu wa kumtuliza.

“Nilihitaji mtu atakayekuwa ananielekeza pale ninapokosea ili nikae sawa, lakini pia mtu ambaye atanijali muda wote, ndio kitu nilichokuwa nikikikosa siku zote.”

MACHO YA UCHEBE YEYE HOI

Kila mtu anacho anachokipenda kwa mwenza wake. Ukimuuliza Shilole nini kinachomvutia kwa Uchebe atakujibu kisha utashangaa.

“Macho ya Uchebe miye hoi bin taabani hasa pale anapocheka. Pia, napenda tabasamu lake ambalo akiliachia meno yake yote huwa hayaonekani,” anasema kisha naye anaangua kicheko.

“Kwa mtu wa kawaida hawezi kuelewa, lakini navutiwa na macho yake hasa anapotabasamu,” anaongeza.

Hata hivyo, Shishi anasema mbali na macho na tabasamu la mumewe, bado anavyo vitu vingine ambavyo vipenda ambavyo hawezi kuvitaja hadharani.

KIKI ZINAMFUATA?

Maisha ya muziki siku hizi ni kiki. Wanamuziki wanapenda sana kiki lakini Shishi kwa upande wake ni tofauti kabisa.

“Sitengenezaji kiki lakini huwa zinanifuata zenyewe. Miaka yangu yote sijawahi kuamini katika kiki lakini nina kismati cha kuandamwa nazo, muziki hauna kiki kikubwa ni kufanya kazi nzuri halafu kiki zitakuja tu.”

Shishi ambaye yuko mbioni kuachia wimbo wake mpya wa Mchakamchaka anaamini wasanii wanaoamini katika kiki wana wasiwasi na kazi zao ndio maana wanaziendekeza.

WATOTO WAKE SAFI TU

Unaweza kudhani labda anachokifanya Shilole kinawaathiri watoto wake lakini siyo hivyo.

“Watoto wangu hawana tatizo na mimi kwa sababu muziki ndio unawalipia wao ada na wanapata wanachokitaka. Nikiwa nyumbani nakuwa mama lakini nikitoka nyumbani nakuwa Shilole, hivyo najitahidi kujitofautisha katika sehemu hizi mbili.”

HATAKI KWENDA ENGLISH KOZI

Eti Shilole huwa anajua Kiingereza vizuri tu, lakini huwa anajichetua akiwa mbele ya kamera.

“Kaka najua kuzungumza vizuri tu Kiingereza na hata kuandika, lakini muda mwingine najifanyisha ili nionekane sijui, kwa hiyo sina mpango wowote wa kusoma English Course kama watu wanajua sijui, basi waelewe kuwa najua vizuri tu,” anasema.

MZIKI WAMPA NYUMBA, APEWA MTAA MAJOHE

Kila mtu anafanya kazi kwa ajili ya kupata mafanikio. Shilole anafichua kuwa muziki umemuwezesha kumalizia nyumba yake iliyopo Majohe Dar. Kwake hicho ni kitu kikubwa ambacho akikiangalia anakuwa anajua jinsi muziki ulivyomlipa katika muda ambao ameufanya.

“Nilianza kuijenga polepole mpaka imekamilika, sasa hivi pale nilipojenga wameanza kupaita kwa Shishi, ukienda Majohe huwezi kupotea kwangu hata kidogo,” anasema.

ANAZICHUKIA TATTOO

Kama wewe unaona ufahari kujichora tattoo, basi kwa Shishi ni tofauti. Kwa sasa anajutia tattoo alizozichora mwilini mwake huku akitamani kuzifuta lakini ndio haiwezekani.

“Nazichukia mno, nilizichora zamani, hapa sijaongeza tena na kama ningempata Uchebe tangu zamani nadhani nisingechora tattoo yoyote lakini ndio hivyo. Huko nyuma nilichora ila sasa nazichukia,” anasema huku akiiangalia michoro hiyo mikononi mwake.

ANAOWAKUBALI

Shilole anafunguka anawakubali Vanessa Mdee, Maua Sama, Khadija Kopa, Nandy na yeye mwenyewe, hiyo ni kutokana na jinsi ambavyo wanatunga mashairi yao.

“Wapo wengi ambao ninawakubali, lakini kwa hawa napenda utunzi wao, mashairi ukiyasikiliza ni mazuri lakini pia hayachoshi.”

ANAPENDA KUJICHANGANYA

Wengi wanaokutana na Shishi kwa mara ya kwanza wanadhani staa huyo ana maringo, lakini hali inakuwa ni tofauti wanapomzoea na kugundua ni mtu wa kawaida.

“Binafsi ni mtu wa kujichanganya kila sehemu, napenda stori na kila mtu na kubadilishana mawazo, lakini linapokuja suala la uongo au majungu huwa nachukia sana, sipendi kuongopewa hata kidogo.”

By THOMAS NG’ITU, Mwanaspoti

Comments

comments


Unataka kutangaza nasi? Tumia namba ya simu hapo chini.

Please contact us: email : info@bongomovies.com or Mobile: +255 756 348 364