Artists News in Tanzania

Shilole, Nuh Wadakwa Gesti Wapelekewa Kituo cha Polisi

Wasanii wa Bongo Fleva waliowahi kuwa wapenzi kisha kumwagana, Zuwena Mohamed ‘Shilole’ na Naftar Mlawa ‘Nuh Mziwanda’ wamekutwa katika nyumba ya kulala wageni kisha kukamatwa na kufikishwa kituo cha polisi kwa madai ya utapeli.

Zilipendwa hao walikamatwa na Jeshi la Polisi wilayani Kahama katika Mkoa wa Shinyanga katika gesti iitwayo Mongo baada ya Nuh kudaiwa kutapeli shilingi milioni moja kutoka kwa promota wa muziki mjini Bariadi katika Mkoa wa Simiyu, Masunga Magembe (Doyer).

Kwa mujibu wa chanzo chetu, Mziwanda na Shilole walikamatwa Januari 21, mwaka huu, majira ya usiku, saa chache kabla ya kupanda jukwaani kuanza kufanya shoo katika Klabu ya Masai, Kahama.

Aidha, ilielezwa na chanzo chetu kuwa, Nuh ndiye aliyekubaliana biashara na Doyer lakini wakati anasakwa, alikutwa na Shilole hali iliyosababisha wawili hao wote kupelekwa kituo Kikuu cha Polisi Kahama Mjini ambapo baadaye polisi waling’amua kwamba Shilole hana hatia hivyo kumuachia huru.

“Shilole walimuachia huru palepale kituoni hivyo kulazimika kufanya mipango ya kumtoa Nuh kwa kuzungumza na Doyer. Doyer akakubali kumuachia kwa ahadi ya Shilole kulipa fedha zote alizokuwa anamdai kesho yake asubuhi,” kilisema chanzo chetu.

Akizungumza kwa simu na gazeti hili juzi juu ya madai ya kutapeliwa na msanii huyo mkubwa nchini, Doyer alibainisha kuwa yeye ndiye aliyefanya mipango hadi kukamatwa kwa msanii huyo.

Doyer alisema walikubaliana na Mziwanda kufanya shoo mjini Bariadi siku hiyo ya Januari 21, 2017 katika Ukumbi wa KMK, lakini ghafla, akashangaa kuona matangazo mengine mitaani, yakionesha msanii huyo atakuwa na shoo nyingine sambamba na Shilole, Kahama Mjini, jambo lililomchanganya kwa sababu tayari walikuwa na makubaliano ya kimaandishi.

Nuh na Shilole wakiwa Stejini, Geita

“Tulikubaliana na Mziwanda Januari 21, kuja Bariadi kwa ajili ya kufanya shoo na nilimlipa fedha za  kuanzia lakini hakutokea na badala yake alikwenda mjini Kahama siku hiyo hiyo kufanya shoo nyingine kinyume cha makubaliano,” alisema Masunga.

Alieleza kuwa walikubaliana kila kitu ikiwa ni pamoja na kumlipa pesa yake ambayo alimtumia Januari 21, asubuhi ambapo alifanya maandalizi lakini baadaye Mziwanda akamweleza kuwa atakuwa na shoo mbili Kahama pamoja na Bariadi.

“Kwa kweli baada ya kuniambia atakuwa na shoo mbili, nilikataa nikamwambia kama ni hivyo rejesha pesa yangu. Hata baada ya maelezo hayo Nuh hakutokea na ndipo nilipotoa taarifa polisi Kahama na kufungua kesi, nikitaka kurejeshewa pesa yangu yote niliyompatia pamoja na gharama za maandalizi,” alisema.

Masunga alieleza zaidi kuwa mara baada ya Mziwanda kukamatwa alikwenda polisi wakafanya mazungumzo, ndipo Shilole akasema yeye atalipa pesa yote na gharama hizo kiasi cha shilingi milioni moja, lakini akaeleza atalipa mara mbili, nusu ya kwanza mara baada ya shoo ya Kahama na nusu ya pili siku moja baada ya shoo.

Kwa mujibu wa Masunga, baada ya makubaliano hayo ya kulipwa fedha zake na gharama za maandalizi, Mziwanda aliachiwa majira ya saa tisa usiku ili kwenda kufanya shoo Masai Club, Kahama.

Hata hivyo, Masunga alidai hadi sasa amelipwa na Shilole nusu ya gharama hizo huku nusu ya pili ikiwa bado haijalipwa na muda wa makubaliano ukiwa tayari umeisha.

“Hadi sasa Shilole amenilipa nusu ya fedha peke yake na kiasi kingine  bado na nimetoa taarifa polisi Shinyanga ambako nimeambiwa Mziwanda na Shilole walifanya shoo juzi Jumapili ili nilipwe kiasi kingine cha pesa,” alisema Doyer.

Gazeti la Amani lilimtafuta Nuh ili kusikia kwa upande wake analielezeaje tukio hilo lakini simu yake ilikuwa tu bila kupokelewa.

Kwa upande wa Shilole, mwandishi wetu alimpigia simu na kumuuliza kuhusu tukio hilo ambapo alijibu kwamba ni kweli walipata matatizo ya kukamatwa lakini tukio hilo linanogeshwa chumvi na mitandao ya kijamii.

“Ni kweli tulipata matatizo lakini tumeshayamaliza, tulikamatwa tukiwa hotelini lakini siyo hivyo kama watu wanavyosema,” alisema Shilole na alipoulizwa hayo yanayosemwa ni yapi, aliishia kusema kwamba tayari wameshayamaliza.

Chanzo:GPL

Comments

comments

Exit mobile version