STAA wa muziki Bongo, Snura Mushi ameibuka na kumkabidhi Makamu wa Rais, Samia Suluhu jipu la wanaume wanaowakataa watoto wao na kuwaachia wanawake mzigo wa kulea peke yao.
Akizungumza na Risasi Mchanganyiko, Snura alisema siku hizi wimbi la wanaume kuwakataa watoto wao ni kubwa sana hivyo tatizo hilo ni sawa na majipu mengine, anamuomba mama Samia alitumbue.
“Namuomba mama Samia kwa sababu ni mwanamke mwenzetu atusaidie kulitumbua hili jipu maana ni kubwa sana yaani tena ni tambazi kabisa, kama rais anavyowatumbua watu naye atumbue hili maana wanawake tumechoka.
“Nina watoto wawili lakini baba zao wamenisusia, wa kwanza alimkataa tangu nikiwa na mimba ya wiki mbili mpaka sasa nalea mwenyewe, huyu mwingine hajawahi kutoa chochote tangu mwanaye huyu azaliwe kitu ambacho kinaumiza sana,” alisema Snura.
Aliendelea kusema kuwa baada ya mama Samia kutumbua hilo jipu anaomba serikali iweke sheria ya kwamba kila kituo cha polisi kiwe kinapokea malalamiko ya wanawake wanaosusiwa watoto au mimba ili shtaka linapokwenda waandikishane na baada ya mtoto kuzaliwa ikigundulika mtoto ni wa mwanaume husika alipishwe fidia.
“Pia kipimo cha DNA kiwepo katika hospitali mbalimbali ili iwe rahisi kupima kwa wale wanaume wanaokataa kwamba watoto siyo wao, sheria hizi zikiwekwa zitasaidia kutokomeza tatizo hilo la watoto kukataliwa na baba zao,” alisema Snura.
Jitihada za kuzungumza na Waziri wa Afya , Maendeleo ya Jamii, Jinsia Wazee na Watoto, Ummy Mwalimu kujua ameipokeaje changamoto hiyo, hazikuzaa matunda kufuatia simu yake kutopatikana hewani.
Snura ni mama wa watoto wawili kila mmoja na baba yake ambapo anawalea mwenyewe huku akikiri kwamba huwa anawaeleza wanaye hao jinsi baba zao walivyowakataa ili baadaye kusije kutokea mvutano wa kimasilahi pindi watakapofanikiwa.
Chanzo:GPL
Comments
comments