Artists News in Tanzania

Ushindi wa Mwana Fa, Ay Umeipa Heshima Sanaa

HARAKATI mbalimbali zinaendelea duniani kote za kuhakikisha kazi za sanaa zinaheshimiwa na kutumika kwa faida ya msanii mwenyewe.

Wakili Albert Msando akiwa na wateja wake, Mwana FA na AY

Habari njema kwenye muziki wa Bongo Fleva ni ushindi wa wasanii Hamis Mwinjuma ‘Mwana Fa’ na Ambwene Yessaya ‘AY’, katika kesi waliyoifungua dhidi ya kampuni moja ya mawasiliano nchini, ambapo jana, Mahakama Kuu ikaitupilia mbali rufaa hiyo na kuitaka iwalipe Sh bilioni 2.18, kufuatia kutumia nyimbo hizo bila makubaliano.

Kesi hiyo ya muda mrefu, iliyochukua miaka mitano toka ifunguliwe na wasanii hao, mwaka jana Aprili 11 kwa mara ya kwanza ilitolewa hukumu na Hakimu Mkazi Mwandamizi, Juma Hassan, katika Mahakama ya Wilaya ya Ilala na kampuni hiyo ikaamuriwa iwalipe Mwana Fa na AY fedha hizo.

Aidha, kampuni hiyo ikafungua kesi ya kupinga kuwalipa fedha hizo, mpaka jana ambapo Mahakama Kuu ikaitupilia mbali rufaa hiyo na kuitaka iwalipe wasanii hao fedha hizo, kwa hiyo Mwana Fa na AY wana uhakika wa kuwa wasanii mabilionea wakati wowote kutoka sasa.

“Ni haki yao kulipwa kwa sababu kazi zao zinalindwa kisheria,” alisema Alberto Msando, ambaye ni mwanasheria aliyekuwa anaisimamia kesi hiyo, iliyozaa hukumu inayokwenda kujenga heshima katika sanaa.

Mwana Fa na AY walifikia makubaliano ya kufungua kesi ya madai dhidi ya kampuni hiyo ya mawasiliano kwa kutumia nyimbo zao mbili, Dakika Moja na Usije Mjini, bila makubaliano katika miito ya simu na mapato yaliyopatikana wasanii hao hawakuambulia kitu.

Sasa heshima itaimarika zaidi katika tasnia, hakuna mdau ambaye anaweza kucheza ovyo na kazi za sanaa na kwa kiasi kikubwa unyonyaji utapungua na wasanii watafunguka macho na kuona umuhimu wa kusajili kazi zao katika Chama cha Haki Miliki (COSOTA).

Sidhani kama Mwana Fa na AY wangeshinda kesi hiyo endapo wasingesajili nyimbo hizo. Kitendo cha wao kuwa wanachama wa COSOTA kimerahisisha kesi na imekuwa na faida upande wao, wasanii fungueni macho zaidi katika hili la usajili.

Unajua unaweza kuwa na haki na kazi yako lakini ukakosa stahiki yako kutokana na kutosajili kazi zako katika vyama vya haki mikili. Wasanii hawa wameonyesha umuhimu wa msanii kusajiliwa katika Baraza la Sanaa a Taifa (Basata) na Cosota.

Mtanzania

Comments

comments

Exit mobile version