‘Ustaa Kwenye Tiba ya Dawa za Kulevya Lazima Tutafeli’
IMEKUWA kama ‘fasheni’ kwa mastaa ambao wanatumia dawa mbalimbali za kulevya kusikia anapata tiba, anaendelea vizuri na kuja na kazi mpya, lakini baada ya muda unasikia amerudia tena kwenye utumiaji wa dawa na inaaminika kuwa nguvu kazi ya taifa inapotea.
Kwanini nasema imekuwa ‘fasheni’, tumeona au kusikia baadhi ya mastaa wameibuka kuwa wanatumia dawa au kupelekwa sehemu maalumu ili kupata masomo, lakini baada ya miezi kadhaa ghafla unasikia karudia tena, mchawi nani? Lazima tufike mahali kama wazazi au wanajamii tunahitaji ndugu zetu wapone kabisa tusimame kidete, tusimame vipi? Kwanini watu wasiokuwa na majina makubwa wapone na wenye majina (mastaa) wasipone, hili swali inabidi tujiulize sana.
Dismas Munishi ni Meneja wa Sober House iliyopo Kigamboni, ikijulikana kwa jina la The Ties That Us Recovery Centre, iliyopo Vijibweni, ameeleza sababu ambazo zinawafanya watu wenye majina makubwa kushindwa kupona na tiba wanazopata.
Sababu za kurudia dawa
Sababu ambazo zinasababisha mastaa hao kurudia kutumia dawa za kulevya pindi wanaporudi uraiani ni ustaa ambao wanauleta wakiwa huko katika nyumba ya elimu, Sober House.
Ubishi wa kupata elimu
Munishi amesema mastaa wengi wanashindwa kupata tiba hiyo kwa usahihi kwa sababu ya ubishi, mara nyingi masomo yanapoendelea wao wanakaa vyumbani na kutaka mwalimu akimaliza kufundisha aende akawafundishe wao peke yao, kwani hawawezi kuchanganyika na waathirika wengine kwa kuwa wao wana hadhi katika jamii.
“Ubishi wa mastaa, kwa kweli wamekuwa wabishi sana, wanatia aibu, hawasikilizi walimu, wengi wamekuwa wakikaa huku bila kupata elimu, hata kama unatumia dawa inabidi upate elimu ya kutosha ili kupambana na kutumia dawa, kwao limekuwa gumu.
Kuishi kistaa
Pia Munishi amesema wanapokuwa katika nyumba hizo wamekuwa wakitaka kukaa kistaa watumikishe wenzao na wao wakiwa hawataki kufanya shughuli yoyote wala kujichanganya na wenzao katika mambo mbalimbali ya jamii, hili limekuwa tatizo kubwa sana.
Usumbufu
Siyo siri katika watu ambao wanasumbua pindi wanapokuwa wakipata tiba basi ni hao mastaa, wanataka wanywe dawa kwa wakati wanaotaka wao bila kujali dawa hizo zina wakati wake, mazoezi pia ni tiba, wanataka waamke muda wanaotaka wao na wakiambiwa sana wanajibu kuwa ikumbukwe wao ni mastaa na wanaheshimika katika jamii, hivyo wana ratiba zao za kulala na kuamka.
Kukatisha matibabu
Mastaa wengi wamekuwa hawamalizi matibabu, kwa kuwa matibabu ya muda mfupi ni miezi minne na mara nyingi hawakai Sober kwa miezi hiyo, wanatoka kabla ya muda.
Wanapoona pale anapoanza kunywa dawa akipata maumivu yale ya masaa 72, hapo tena basi anajua amepona kabisa, wakati si kweli. Ndani ya miezi hiyo minne anajifunza vitu vingi, ikiwemo kupewa masomo ya ushauri na jinsi ya kujikinga, sasa wao ikifika mwezi mmoja au miwili basi wanashindwa kabisa kuvumilia na kujifanya wana mambo mengine nje.
Kushindwa kuukubali ukweli
Wengi wao huwa hawakubali ukweli, hawakubali kuwa wameshadhalilika sasa wanahitaji kurudisha heshima ndani ya jamii, wao wanadhani kuvuta madawa ndiyo kurudisha heshima na muziki wake kukubalika, kitu ambacho si kweli, na hilo ndilo limekuwa likitupa changamoto katika utoaji elimu, ndipo ambapo tunaamini mtu akifanikiwa kumaliza matibabu kwa miezi minne anaweza kuwa sawa.”
Anamzungumzia Ray C
“Ray C ni mmoja wa mastaa ambao tulikuwa nao hapa, yeye alikuwa katika Sober ya Pederef (Nuru Sober House) iliyopo Vijibweni, Kigamboni.
“Ni mmoja wa mastaa wabishi sana, kwa hali hiyo anaweza kuzidi kuwa katika wakati mgumu kutokana na tabia hiyo. Aliondoka hapa bila kumaliza dawa, walimshindwa Bagamoyo kwa sababu kama alizokuwa anafanya hapa, ustaa mwingi na bado hajaukubali ukweli.
“Alikuwa mvivu kuhudhuria darasani akitaka afundishwe peke yake na mambo mengine kama hayo, ambayo yanafanya staa akitoka huko kushindwa kuidhibiti hali ya utumiaji dawa za kulevya kwa kuwa anakuwa hajapata tiba yote,” alisema.
Ushauri
Ndugu na jamii ambayo inawapeleka mastaa katika nyumba hizo na kulipa pesa zao ili watu hao waachane na dawa hizo na kurudi katika maisha yao kama zamani, wanatakiwa wawafuatilie kwa kina na kuhakikisha hata wakiwa katika nyumba hizo basi wanafuata masharti kama wanavyofanya watu wengine ili kuepuka tabia ambayo imezoeleka ya kurudia katika uvutaji wa dawa hizo.
Mtanzania