Vee Money Afungukia Kukutana na Michelle Obama
Oktoba 11, ilikuwa ni Siku ya Msichana Duniani, ambapo jarida maarufu Marekani, liitwalo Glamour, lilifanya majadiliano maalumu yaliyopewa jina la Brighter Future: Global Conversation On Girls’ Education ambapo ‘first lady’ wa taifa hilo Michelle Obama alizungumza na wasichana duniani kote kuhusiana na umuhimu wa elimu kwa mtoto wa kike kupitia njia ya mtandao.
Kwa upande wa Bongo, mwanamuziki wa kike, Vanessa Mdee ‘Vee Money’ aliliongoza kundi la wasichana 25 ambao ni wanafunzi kutoka shule za sekondari mbalimbali nchini katika mjadala huo wakiunganishwa na Michelle, kutoka kwenye ubalozi wa Marekani nchini.
Baada ya mjadala, hivi karibuni akizungumza na Uwazi Showbiz kuhusu namna alivyopata shavu hilo la kuwasindikiza wasichana hao kuzungumza na Michelle alisema:
“Shavu hilo nililipata kutoka serikalini kwa sababu kwanza mimi ni mtoto wa kike, lakini nimefanya kazi za kijamii sana zikiwemo za kupigania haki za wasichana. Lakini kuhusu Michelle kukutana naye kupitia mtandao kumefanya nijifunze mengi, kwanza ni mwanamke jasiri na sikuwahi kufikiri kama anaijua Tanzania na Afrika kwa namna alivyoizungumzia, zaidi amenitia moyo kuendelea kupigania haki za wasichana.”
Mastaa wengine duniani walioshiriki kwenye mdahalo huo kutoka kwenye nchi zao ni pamoja na Muigizaji Rowan Blanchard (Marekani), mtangazaji kutoka Peru, Mavila Huertas na Mtangazaji Mais Nobani (Jordan).
Chanzo:GPL