Waganga Watanimalizia Pesa – Dully
Msanii mkongwe wa muziki wa Bongo Fleva, Prince Dully Sykes amefunguka na kusema kwamba wasanii au watu wanaokwenda kwa waganga wa kienyeji ili kufanikiwa wanaongozwa tu na tamaa na kutoridhika na kile wanakichopata.
Dully amefunguka hayo alipokuwa kwenye Planet Bongo ya East Africa radio ikiwa ni siku chache baada ya Meneja Maneno kufunguka na kudai wasanii wengi wanaaminmi ushirikina na kusema kwamba yeye hawezi kufanya hivyo kwani anaridhika na maisha yake kwa kila akipatacho.
“Mimi maisha yangu naridhika nayo japo si makubwa kiivyo, naridhika na kagari ambacho naendesha, naridhika na mahali ninapolaza ubavu wangu, naridhika na chakula ninachopata, ninaridhika na kipato ninachopata japo ni kidogo ila nagawana na wenzangu, watoto na familia,” amesema Dully Sykes.
Dully ameongeza kuwa “Sifikirii kama kuna mganga ambaye anaweza kufanya mimi nikapata hela zaidi ya hapa, sana sana watanimaliza hela zangu,” ameongeza.
EATV.TV