Artists News in Tanzania

Wagosi wa Kaya na Mwanzo Mpya Katika Muziki

WAGOSI wa Kaya ni moja ya makundi yaliyoweka historia mkoani Tanga wakitambulika na Kibao cha Tanga Kunani na baada ya hapo wakawashika mashabiki vilivyo na vibao vingine kama Wauguzi, Tajiri na Maskini, Pole, Trafiki, Kibaka Kaokoka na Taxi Driver.

Kundi hilo linaloundwa na vichwa viwili, John Evans ‘Dk. John’ na Fredy Mariki ‘Mkoloni’ limefanikiwa kwa kiasi kikubwa kutengeneza staili ya aina yao katika Muziki wa Bongo Fleva mmoja akiimba Kisambaa na mwingine Kidigo. Katika makala haya, Ijumaa limefanikiwa kukutana na wakali hao ambao kwa sasa wameungana na kurudisha kundi baada ya kufanya muziki kila mtu kivyake kwa muda mrefu.

Kwa mujibu wa Dr. John anaeleza kuwa moja ya sababu zilizowafanya kurudi upya kwenye gemu ni kupoteza mashabiki wengi ambao walitamani kuwaona kama kundi na siyo mmojammoja.

Ijumaa: Changamoto zipi mmekutana nazo baada ya kurudi tena kwenye muziki?

Wagosi: Zamani tulikuwa tunapata pesa kwenye shoo na mauzo ya albamu lakini sasa pesa inapatikana zaidi kwenye shoo. Sasa hivi mtu yupo tayari kuingia mtandaoni na kupakua nyimbo zako bure tu. Ulipwaji wa shoo wa siku hizi tofauti na zamani.

Unajua muziki wa zamani mlikuwa mkitoa wimbo DJ anataka kuwa wa kwanza kuutambulisha lakini siku hizi kuna utofauti mkubwa. Kwanza uingie kwenye magazeti, redio, TV na mitandao ujitangaze bila hivyo watu hawajui unafanya nini.

Ijumaa: Tungependa kujua kifamilia zaidi, mna watoto wangapi?

Wagosi: (Dr. John) Kwangu mimi kama mashabiki wanakumbuka miaka mitatu iliyopita nilifiwa na mke wangu niliyezaa naye watoto wanne wote wa kike.

Hata hivyo, baada ya miaka miwili nikafunga ndoa tena, kwa upande wa Mkoloni ana mke na watoto wawili wa kiume na kike.

Ijumaa: Kimuziki sasa, mmejipangaje kimataifa? Maana Bongo Fleva kwa sasa imetanuka tofauti na zamani.

Wagosi: Huko ndipo tunapoelekea na ujio wetu huu tumeanza kuchokoza kwanza nyumbani kuwakumbusha mashabiki wetu. Video tumeshaanza mipango ya kutengeneza zile zenye hadhi ya kimataifa na hata kolabo tunatarajia kufanya za kimataifa kwanza.

Ijumaa: Kuna mipango yoyote ya makubaliano ya kolabo na staa wa kimataifa?

Wagosi: Hivyo bado hatuwezi kuviweka wazi kwa sasa vipo kiuongozi zaidi, ila tunapenda sana kufanya kazi na magwiji wenzetu kutoka Marekani mfano Snoop Dogg.

Ijumaa: Aina ya muziki mnaofanya, zamani ulikuwa na mapokeo makubwa sana vipi kwa sasa? Wagosi: Mashabiki wapo, Wagosi kama Wagosi wakikaa kimya nyuma kuna mashabiki wake nao wapo kimya.

Ujue hawa wanamuziki wengine wanaoimba ukiwachunguza utaona wanafanana sana, sasa Wagosi kama Wagosi kuanzia mashairi jinsi ya kupeleka ujumbe kwanza unacheka, unapata ujumbe na unaburudika, hiyo ndiyo staili yetu. Hakuna yeyote aliyejitokeza kwa miaka 10 tuliyokuwa kimya akafanya staili yetu.

Hata ujio wetu huu mpya ni kelele za mashabiki kutumisi. Mapokeo zamani wasanii walikuwa wakihesabika mfano Nature, Gangwe Mob, Daz Nundaz, Prof Jay na ndiyo haohao kwenye shoo lakini siku hizi watu wanafanya kweli kuimba wanaimba sana.

Miziki ya zamani sasa hivi ukiileta huwezi kutoboa, sasa hivi madogo wanaimba yaani wanaimba kweli. Sisi tumegundua kipindi hiki nini mashabiki wanataka ndiyo maana tumeamua kubadilika.

Ijumaa: Tumezoea kuwaona wawili tu, kutokana na ushindani uliopo kwenye muziki labda mna mpango wowote wa kuongeza nguvu (mtu) kwenye kundi lenu?

Wagosi: Kuna dada yetu anaitwa Amara ambaye ni kama ‘first lady’ wa Wagosi, tumemshirikisha katika wimbo wetu mpya wa Upepo Siyo. Kwa muda amekuwa akitambulika sana Tanga katika bendi tofauti. Tunamtangaza lakini Wagosi hatuna mpango wa kumuongeza mtu zaidi ya kuwashirikisha.

Ijumaa: Kuna wakongwe wengi mliokuwa nao wanashindwa kurudi kwenye gemu, wanapiga nyimbo mbili tatu wanakata tamaa na kuacha muziki, mnaona tatizo ni nini?

Wagosi: Muziki unatakiwa uwe na mambo mengine ya kufanya. Pia hauhitaji kuupania utakukataa tu, unatakiwa uufanye kama vile hutaki kumbe ndiyo unafanya.

Siyo ukitoa singo leo unataka kesho pesa iingie hapana! Unatakiwakuwa na subra, unafanya utaona shoo haziji we’ endelea kufanya tu. Wengine wanakata tamaa utakuta video bei kali, milioni tatu huko ukiangalia hana meneja.

Gemu la sasa hivi unatakiwa ulisome kwanza kama ulikuwa ukifanya zamani unatakiwa urekebishe sehemusehemu kimashairi.

Ijumaa: Mna mpango wowote wa kuingia kwenye siasa kama wakongwe wenzenu walivyowatangulia, Sugu na Prof. Jay?

Wagosi: Hatuna mpango huo. Ila ikitokea wahamasishaji wakatufuata na kutuomba hatuwezi kukataa, hata hao wasanii walioko kwenye siasa leo hii kuna watu nyuma yao waliwafuata na kuwaomba kugombea.

Chanzo:GPL

Comments

comments

Exit mobile version