Wastara Aelezea Mpasuko Kwenye Fuvu la Kichwa
Msanii wa filamu nchini Wastara Juma amefunguka na kudai baada ya kufanyiwa vipimo vyote nchini India amebainika kuwa na tatizo kwenye fuvu lake la kichwa ambapo hilo ndio lililokuwa likimfanya akose usingizi hapo awali bila ya yeye kujitambua.
Wastara ameeleza hayo mara alipowasili katika ardhi ya Tanzania akiwa anatokea nchini India ambako alienda kufanyiwa matibabu ya mguu pamoja na mgongo uliyokuwa unamsumbua kwa kipindi kirefu lakini baada ya kufika huko alikutwa na matatizo mengine tofauti na hayo.
“Ni tatizo ambalo lilikuwa linahitajika kuchukuliwa umakini kwa sababu muda mwingi nilikuwa nalalamika kukosa usingizi, kitu ambacho mimi mwanzo nilikuwa nadhani labda ni kutokana na mawazo niliyokuwa nayo lakini siyo hivyo. Kwenye fuvu la kichwa kuna mpasuko kwa nje na kusababisha kama uvimbe jambo ambalo lilikuwa linanisababishia kukosa usingizi”, amesema Wastara.
Pamoja na hayo, Wastara ameendelea kwa kusema “nimefanikiwa kupata dawa pia na ninatakiwa nitumie kila baada ya miezi mitatu na kama kuna uwezekano wa kupata matibabu hapa hapa nchini itakuwa vizuri. Wenyewe wamenishauri kama itawezekana niweze kupata bima ya afya kubwa kwa sababu kama kuna ulazima wa kurudi kila baada ya miezi mitatu iwe rahisi ili niweze kuangalia tatizo la kichwa kwa sababu sio jambo la kulifanyia masihara”.
Kwa upande mwingine, Wastara amesema anamshukuru Mwenyezi Mungu kwa kumuwezesha kurudi salama nchini pamoja na tatizo lake la mguu linaendelea vizuri japokuwa bado yupo kwenye uangalizi.