Waziri Mwakyembe Awamwangia Sifa Bongo Movie
WAZIRI wa Habari Utamaduni Sanaa na Michezo Dkt. Harrison Mwakyembe amepongeza shirikisho la filamu na wadau wake kufuatia kufanikiwa kusajili mfuko wa filamu pamoja na mikakati ya muda mrefu na mifupi, akiongea na wajumbe wa Bodi ya Taff na wadau chini ya Bodi ya Filamu amesema kuwa amefarijika sana kupokea taarifa za Tasnia ya filamu.
Akimkaribisha Mh. Waziri katibu mtendaji wa Bodi ya Filamu Tanzania Bi. Joyce Fissoo alianza kwa kutoa wasifu wa wajumbe wanaounda mfuko huo ambao ni Jack Stephen Gothan (Mwenyekiti), Asha Dodo Mtwange, Prof. Amandina Liamba, Masoud Ali ‘Masoud Kipanya’, na Sauda Simba pia katibu alitaja majina mawili ya wadau wa filamu.
Majina yaliyongezewa ni Adam Juma akiwakilisha chama cha wapiga picha na mjumbe wa Bodi ya Taff Irene Sanga mjumbe wa Bodi ya filamu ambao wameongezwa kufuatia kikao kilichofanyika katika kuongeza wadau ndani ya mfuko unaojulikana kama Taff Trust fund.
“Mheshimiwa hapa katikati kulikuwa na migogoro kweli kweli jana tulikuwa na kikao tulisema kweli nikuhakikishie tumemaliza salama na watu wakaondoka wakifurahi na kugongesha chupa za vinywaji hakuna ugomvi,”alisema Bi. Fissoo.
Baada ya katibu ambaye ndio alikuwa msimamizi na mwenyekiti wa kikao hicho alimkaribisha katibu wa mfuko Bi. Asha kuelezea malengo ya muda mfupi na muda mrefu, yahusuyo mfuko ambao wanaamini kuwa ndio itakuwa mkombozi wa wadau wa tasnia filamu kutokana na kukosa dhamana katika taasisi za kifedha.
Pamoja na malengo makuu lakini iliwapasa Taff kusajili mfuko wa filamu kwa sababu Taff ni taasisi ambayo hairuhusiwi kufanya biashara zaidi ya kuangalia masula kama ya Sera, Uzengezi, kuwajengea uwezo kwa wadau wake, kulinda haki zao na utetezi wa haki zao kwa mantiki hiyo moja kati ya kazi ya mfuko kuwasaidia wadau.
Mikakati ni kujenga mji wa sinema ambao utajulikana kwa jina la Waswahili City ambao utajengwa katika wilaya Bagamoyo, kuwa na kampuni ya uzalishaji wa filamu , kutoa mikopo kwa wadau wa filamu kutoa Elimu kwa watengenezaji wa sinema.
Waziri alisema kuwa anawapongeza sana wasanii wa filamu kwa juhudi zao ambazo ameziona hasa kwa kusajili mfuko ambao pengine hakuna shirikisho lingine ambalo limefanya hivyo ambapo aliongea na wasanii wa Bongo fleva waanzishe mfuko ambao utasaidia wasanii kufanikisha kazi bora na kuwaletea maslahi.
“Kwanza nikushukru sana katibu mtendaji, katibu wa mfuko na wajumbe, niwapongeze kwa uamuzi mliochukua kuwa na mfuko ni kitu ambacho kilikuwa hakipo, kwa upande wangu tatizo lilo kubwa na linakwamisha wasanii wetu wa filamu kama wengine ni ukosefu wa mitaji,”Dkt. Mwakyembe.
Waziri alisema kuwa kukosekana kwa mitaji kumewaingiza vijana wengi katika mtego wa mikataba mibovu na matajiri wachache ukiangalia mikataba mingi imejaa unyonyaji wa hali ya juu kabisa, kutokana na unyonyaji uliopo katika mikataba hiyo hakuna msanii au mdau ambaye anaweza kutoka katika umaskini kwa kuuzwa kwa kazi yake.
“Nimefarijika sana kwa hizi juhudi mlizozionyesha kuwa na mfuko wa filamu, kwa juhudi hizi zinanifanya kuona hata nikiondoka kuna kitu kimefanyika pale nimefurahi sana, kuwepo kwa mfuko huu na mimi ni mwanachama,”
Aidha katika kuonyesha kuguswa na dhuluma iliyowakuta wadau wa filamu Mh. Waziri anaona kuna sababu ya kupitia mikataba yote ya nyuma ambayo kuna baadhi ya wasanii waliingia kwa kushindwa kujua unyonyaji uliopo katika mikataba hiyo ambayo ilitayarishwa na wasambazaji ambao walikuwa na madalali wa kazi zao.
“Haiwezekani mtu kauza kazi ambayo hana umiliki anashindwa hata kununulia shati tu, na mmiliki asiye haki awe ndio mwenye haki hilo haliwezekani ngoja kwanza vumbi litulie tutaifanyia kazi,”
“Pia kuhusu suala la mfuko unahitajika sana wasanii wote hamkopeshiki nyinyi wenyewe mmesema na siyo kwa sababu ya sura zenu hapana vijana mnapendeza maridadi kabisa shida mliyokuwa nayo tasnia haiaminiki na mikataba yenu mnayoingia pia haiaminiki,”alisema Dkt. Mwakyembe.
Dkt. Mwakyembe alitumika msemo wa Kiswahili kuwa mkono mtupu haulambwi, hivyo kuwaimiza wasanii na wadau wa filamu kuanza kwa kuchangia kila mdau mnufaika na mfuko huu kwa kutoa kiasi cha 1,000 kwa kila mwezi ambapo ni wastani Tshs. 12, 000 kwa mwaka iwapo italipwa kwa wakati ni sawa Bilioni 36.
Mfuko huo unatarajiwa kuziinduliwa rasmi kabla ya mwaka ujao kwa utekelezaji wa maombi ya Mh. Dkt. Mwakyembe kuwa ifanyike utaratibu wa kuchangiwa na wasanii na wadau wa filamu wanaokisiwa kuwa zaidi ya milioni 3, Kikao cha wadau na Mh. Waziri kilifanyika katika hoteli ya Court Yard iliyopo Upanga na kushirikisha wajumbe wa Bodi ya filamu.
Filamucentral