Wema Amuachia Mungu Swala la Kupata Mtoto
STAA mwenye jina kubwa nchini katika Bongo Movie, Wema Sepetu amesikia kauli za mashabiki wake kuhusu kushindwa kupata mtoto mpaka sasa, lakini amewaambia hata yeye anaumia, ila hajakata tamaa kuitwa mama.
Wema alisema sio kama hajahangaika au eti ameridhika kuishi bila mtoto, isipokuwa jitihada zake zimekwamishwa na bahati na sasa ameamua kumwachia Mungu amfanyie miujiza kwa kutambua kuwa yeye ndiye kila kitu hapa duniani.
“Si kila kitu kinaweza kuwa hadharani, lakini nimeanza kuusaka ujauzito nikiwa na miaka 24, kila nikifanya hivyo mambo hayawi sawa hilo jambo sipendi sana kumsikia mtu akijadili kwani linaniumiza sana,” alisema Wema.
Aliongeza kuwa, yeye kama mwanamke, anatamani naye kuitwa mama kwani mtoto wake ni tofauti na wa mwingine, lakini ni mipango ya Mungu na kuna wakati binadamu inampasa kukubaliana na mapito na kumwachia Mungu.
“Ninatamani sana mtoto, watu wakinisakama kana kwamba ninayapenda haya, ila naamini iko siku chozi litafutika.”
Mwanaspoti