Wema Awekwa Chini ya Ulinzi
Mama kijacho Wema Abraham Sepetu ‘Madam’ kwa mara nyingine ametengeneza kichwa cha habari, safari hii amewekwa chini ya ulinzi wa polisi kwa kosa la kuendesha gari aina ya Range Rover Evogue bila kuwa na vibali, Risasi Jumamosi lina ‘full’ stori.
Tukio hilo lililodumu kwa takriban saa tatu lilijiri Jumanne iliyopita maeneo ya Aficana, Mbezi Beach jijini Dar wakati mrembo huyo alipokuwa ‘kiguu na njia’ kwenda kwenye bethidei ya rafiki yake aliyefahamika kwa jina la Kibadude.
NI LILE ALILODAI KUJIZAWADIA
Kwa mujibu wa chanzo makini kilichokuwepo eneo la tukio, gari hilo alilokamatwa nalo Madam ni lile alilojizawadia kwa mbwembwe nyingi mwishoni mwa mwaka jana katika siku yake ya kuzaliwa ambalo lina thamani ya shilingi milioni 200 za Kibongo.
“Nimepiga picha. Wamemtaiti hapa Mbezi Africana, naona maofisa wa TRA wanamhoji. Lina tatizo katika uhalali wa kuingia nchini. Hapa sasa naona wanaomhenyesha ile mbaya. Si kawaida.”
AMWAGA CHOZI
“Sasa namuona Madam machozi yanamtoka yenyewe… anahaha, mara aende huku mara kule. Nahisi so litakuwa limemkalia vibaya maana kila simu anayopiga hapati msaada,” kilinyetisha chanzo hicho.
TRA WABAINI FIGISUFIGISU
Gazeti hili lilizungumza na ofisa mmoja wa TRA ambaye alikuwepo kwenye tukio hilo aliyeomba hifadhi ya jina kwa kuwa si msemaji wa mamlaka hiyo aliweka wazi kuwa, walibaini figisufigisu katika gari hilo.
“Hili gari ni moja kati ya magari ambayo yanaingia nchini kutokea nchi ya Msumbiji. Hata namba zake za usajili zinaonesha hivyo. Sasa huwa yanakatiwa vibali vya miezi mitatu au kulipiwa ushuru na kununuliwa. Liliingia nchini tangu mwaka jana.
“Tumekuta halina vibali maana vibali vya miezi mitatu vimeisha, tumemuuliza atoe nyaraka za gari, anasema zipo nyumbani, tukamwambia twende huko nyumbani ukazitoe, akabadili lugha, akasema anazo Steve (Nyerere). Inaonekana hili gari lina matatizo makubwa ya ushuru,” alisema ofisa huyo.
FIGISU NYINGINE
Kumbukumbu zinaonesha gari hilohilo la Wema ambalo alisema amejinunulia kwa fedha zake, ndilo alilodaiwa kununuliwa na mbunge machachari wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) ambaye aliwahi pia kutajwa kuwa ndiye baba kijacho wake kabla ya Idris Sultan kuibuka na kujinadi kuwa ndiye ‘mmiliki’ halali wa tumbo hilo.
KIGOGO SERIKALINI AMUOKOA
Paparazi wetu alimtafuta mtu wa karibu kabisa na Wema ambaye alieleza kuwa, Madam baada ya kuhaha kwa muda mrefu eneo hilo huku akiwa chini ya ulinzi wa polisi wenye bunduki, alipata wazo la kumpigia kigogo mmoja serikalini (jina tunalo) ambaye alimpa msaada kwa masharti.
“Alimpigia simu… (anataja jina la kigogo), akamweleza matatizo yaliyomkuta, naye akazungumza na maofisa wa TRA, wakakubaliana kwa masharti kwamba asilitumie gari hilo ndani ya wiki moja mpaka apeleke vibali vya gari hilo,” alisema mtu huyo wa karibu na Wema.
HUENDA LIKATAIFISHWA KAMA LA WOLPER
Kwa mujibu wa taratibu na sheria za TRA, endapo Wema atashindwa kutoa nyaraka muhimu za gari hilo hatua za kisheria zitachukuliwa dhidi yake ikiwa ni pamoja na kutaifishwa kwa gari hilo kama ilivyomtokea mwigizaji Jacqueline Wolper ambaye mwaka 2014, gari lake aina ya BMW X6 lilikamatwa na kutaifishwa kwa kushindwa kulipia ushuru na kukosa vibali halali.
WEMA ASAKWA
Baada ya kupewa taarifa hizo, gazeti hili lilimtafuta Wema kwenye simu yake ya mkononi lakini muda wote iliita bila kupokelewa na hata alipotumiwa ujumbe mfupi, hakujibu.
MENEJA WA WEMA ANENA
Alipoulizwa kuhusu suala hilo, meneja wa msanii huyo, Martin Kadinda alisema yeye alisikia kwa watu kuhusu taarifa za Madam kukamatwa na gari hilo lakini alipomuuliza alimwambia si kweli, ni uzushi tu na hata gari hilo lipo nyumbani aende kuliona jambo ambalo alilifanya na kweli akajionea gari hilo.
“Ni uzushi tu. Nimeongea na Madam, akanihakikishia kwamba hamna kitu kama hicho. Nikaenda kulitazama gari, nikalikuta nyumbani kwake Ununio, shwari kabisa,” alisema Martin.
Gazeti ndugu na hili, Amani, toleo la Alhamisi iliyopita, ukurasa wa nyuma kulikuwa na habari yenye kichwa; Range la Wema layeyuka. Msingi wa habari hiyo ni taarifa kuwa, Wema haonekani akiwa na gari hilo licha ya kujinadi kuwa ni lake. Amekuwa akitumia kigari kidogo ‘ki-kirikuu’ kuendea kwenye shughuli zake.
Ilidaiwa kuwa, Wema alilipeleka gereji au yadi ya kuuzia magari, gari hilo hali iliyowafanya mapaparazi wa OFM kulisaka bila mafanikio huku ikielezwa kuwa, gari hilo si lake bali huwa anapepewa kwa muda kujiachia nalo.
Chanzo: GPL