Wema, Diamond masaprize kibao
JUZI Jumapili wakati watu wakisherehekea Sikukuu ya Pasaka kwenye kona mbalimbali za kula bata, wadau wa Sanaa nchini wakiwemo wasanii wenyewe walikuwa pale Mlimani City, Dar es Salaam, wakifanya yao.
Kwa baadhi ya wasanii ilikuwa ni bonge la saprize iliyojaa furaha pale walipotangazwa kuwa washindi kwenye tuzo za filamu za Sinema Zetu International Film Festival Award (SZIFF).
Tuzo hizo ziliandaliwa na Azam Tv kupitia chaneli ya Sinema Zetu kwa lengo la kutambua kazi za wasanii wa tasnia hiyo, ambapo viongozi mbalimbali walihudhuria akiwemo Rais wa Awamu ya Nne, Jakaya Kikwete.
Katika tuzo hizo jumla ya vipengele 19 vilishindaniwa, ambapo washindi waliondoka na zawadi mbalimbali ikiwemo mkwanja kuanzia Sh2 milioni hadi Sh5 milioni kwa msanii bora wa kike, wa kiume na muongozaji bora wa filamu.
Malkia wa Bongo Movie, Wema Sepetu ambaye alikuwa kivutio kikubwa kwenye tuzo hizo, alishinda kipengele cha Mwigizaji Bora wa Kike wakati Mwigizaji Bora wa Kiume ni Salim Ahmed huku Mwongozaji Bora tuzo yake ikienda kwa Daniel Manege, ambaye ameongoza filamu ya Safari ya Gwalu.
Mondi, Mobeto gumzo
Pamoja na kuwepo kwa matukio mbalimbali katika shughuli hiyo, utamu ulinoga zaidi pale staa wa Bongo Flava, Naseeb Abdul ‘Diamond’ alipoungana na mzazi mwenzie, Hamisa Mobeto katika kukabidhi tuzo kwa mshindi. Wawili hawa wamekuwa kivutio kutokana na hivi karibuni kuingia kwenye mgogoro wa matunzo ya mtoto wao, Dillan hadi kufikia kupandishana mahakamani. Hata hivyo, juzi katika utoaji wa tuzo hizo, Diamond ambaye alikuwa wa kwanza kuitwa jukwaani kukabidhi tuzo na baadaye mshehereshaji kumuita Mobeto katika kuungana na msanii huyo. Hiyo mbali ya kuwa saprize kwa wawili hao, pia iliwahusu mashabiki ambao hawakuwa wakitarajia hilo kutokea.
Hivyo katika kipengele cha ‘Best Original Music’ kumbe walipangiwa Mobeto na Diamond kukabidhi tuzo hizo, ambapo ilipofikia zamu ya kutangazwa kwa mshindi alianza kuitwa Diamond jukwaani na hapo ukumbi ukalipuka kwa furaha. Muda mfupi baadaye mshehereshaji alitaja jina la Mobeto kuwa ndiye atakayeungana na Diamond, jambo lililozidi kulipua ukumbi kwa kelele za shangwe ambapo, mrembo huyo naye hakufanya kosa kwani alipanda jukwaani kwa madaha akiwa amevaa gauni lake jeupe lilibana vizuri mwili wake na kuongeza mvuto.
Alipofika kwenye ngazi, mshereshaji wa kike alimshika mkono wakati akipanda ngazi na kumkabidhi kwa Diamond, ambaye alimkumbatia na kuongeza kelele ukumbini huku kila mtu akisema lake.
Baada ya hapo Diamond alizungumza maneno machache ya shukurani ambapo, alidai kuwa amefurahishwa na tuzo hizo kwa kuwa zimemuwezesha kukutana na mzazi mwenzie, jambo ambalo lilisababisha tena ukumbi kulipuka kwa shangwe.
Diamond, ambaye amekuwa gumzo kwa sasa, hakuishia hapo alimwagia sifa Mobeto kwa namna alivyopendeza na alipomaliza hapo alimwonesha karatasi Mobeto ili aweze kumsoma mshindi na ndio hapo akaitaja filamu ya ‘Safari ya Gwalu’ kuwa ndio imeshinda kipengele hicho cha ‘Best Original Music’.
Baada ya kumaliza kufanya hivyo, Diamond alimshika Mobeto na kushuka naye jukwaani na kisha kwenda kumsalimia Rais Mstaafu, Jakaya Kikwete.
Wema afunguka
Akizungunguzia tukio hilo, alipotakiwa kutoa maoni yake, Wema, ambaye chupuchupu tuzo hiyo iende kwake kupitia ya ‘Heaven Sent’, kutokana na kuwa moja ya filamu iliyoingia kwenye kipengele hicho, alieleza kuwa tukio hilo ni la kawaida. Wema, ambaye amewahi kuwa mpenzi wa Diamond na sasa ikielezwa kuwa uhusiano wao umerejea tena kwa kasi baada ya Zari kubwaga manyanga, amesema anamchukulia kawaida kwa Mobeto na Diamond kwa kuwa ni mtu na mzazi mwenzake.
“Wee ulitaka nichukuliaje labda, Mobeto na Diamond hawa ni wazazi na mimi na yeye ni ushkaji tu,” amefunguka.
Baadhi ya washindi
People Choice Award)- Heaven Sent
Filamu Bora- Safari ya Gwalu
Muongozaji Bora- Daniel Manege:- (Safari ya Gwalu )
Muigizaji Bora wa Kiume- Salim Ahmed ( Gabo)
Muigizaji Bora wa Kike- Wema Sepetu
Mchekeshaji Bora- Musa Kitale
Best Screen Play:- Safari ya Gwalu (Daniel Manege)
Mhariri Bora- Watatu Carole Gikandi Omondi)
Best Original Music:- Safari ya Gwalu
Best Cinematography:- Watatu
Kwa filamu fupi
Filamu bora – Binti Zanzibar
Muongozaji Bora- Said Abdallah Haruni (Picha)
Best Screen Play:- Binti Zanzibar (Barke Ali Muhsin na Salum Maulid Stika).
Mwananchi