Chupuchupu! Mwanadada anayeng’ara kunako tasnia ya filamu za Kibongo, Jacqueline Wolper, juzikati almanusra apigwe risasi kwenye kituo kimoja cha mafuta kilichopo Tegeta (jina linahifadhiwa) jijini Dar es Salaam, baada ya kuibuka kwa timbwili zito eneo hilo, Risasi Mchanganyiko linakupa mkasa mzima.
Tukio hilo la aina yake, lilijiri mishale ya saa tano usiku wa Juni 12, mwaka huu ambapo kwa mujibu wa chanzo chetu cha kuaminika, Wolper alinusurika kupigwa risasi na mlinzi wa kituo hicho cha mafuta baada ya kutokea hali ya sintofahamu kati yake na mfanyakazi mmoja kwenye kituo hicho.
“Ishu yenyewe ni kwamba, kuna muda Wolper alifika pale sheli (Sheli ni neno lililozoeleka likimaanisha kituo cha mafuta, lakini ukweli ni kuwa jina hilo ni la kampuni ya mafuta yenye makao makuu yake Nchini Marekani) akiwa ndani ya gari aina ya Toyota Mark X, lile linalodaiwa kuwa ni la mpenzi wake wa sasa, Harmonize (Rajab Abdulkan).
“Akaongeza mafuta na kuondoka zake, dakika kadhaa baadaye, tulishangaa kumuona Wolper akirudi tena na kwenda mpaka kwa yule dada aliyemuuzia mafuta lakini safari hii alionekana kuja kwa shari.
“Akashuka kwenye gari na kuanza kumuwakia yule dada kwa madai kwamba amemuibia mafuta na kusababisha gari lake limzimikie njiani wakati alitoa shilingi elfu ishirini,” kilisema chanzo chetu.
Kwa mujibu wa chanzo, timbwili la aina yake lilizuka eneo hilo baada ya msichana huyo kuanza kumjibu mbovu msanii huyo ambaye hakukubali, Wolper akakinukisha kwa kumvaa na kuanza kumshushia kichapo, tukio lililokusanya umati wa watu.
Ilibidi mlinzi wa kituo hicho cha mafuta, aingilie ugomvi huo. Hata hivyo, mlinzi huyo alionekana kumtetea zaidi mfanyakazi mwenzake na kumkandamiza Wolper, jambo lililozidi kumpa hasira msanii huyo.
“Alipoona wanasaidiana, Wolper aliwachenjia wote wawili, jambo lililosababisha mlinzi huyo aondoke eneo hilo lakini aliporejea, alikuwa na bunduki yake ya lindo mkononi, akaikoki na kutaka kumpiga risasi Wolper,” kilisema chanzo chetu na kuongeza kuwa kuona hivyo, Wolper alikimbilia ndani ya gari lake na kutoka nduki, akiacha watu wengi wakiwa wamekusanyika kituoni hapo.
Baada ya kusikia maelezo hayo kutoka kwa chanzo chetu, Risasi Mchanganyiko lilimtafuta Wolper ambaye baada ya kusomewa mashtaka hayo, alikiri kutokea kwa tukio hilo.
“Dah, ni kweli nilikutana na matatizo hayo usiku, ambapo nilikuwa naenda Tegeta baada ya kufika njiapanda flani pale, gari lilipungua mafuta nikaingia kituoni na kuongeza ya elfu 20, wakati naongeza nilihisi kabisa yule dada ananiibia lakini sikumjali, nikalipa na kuondoka.
Nilipofika mbele kidogo tu gari lilizima,” alisema Wolper na kuongeza: “Ilibidi nifanye utaratibu wa kupata mafuta mengine kisha nikageuza na kurudi mpaka pale sheli kwa lengo la kudai haki yangu ndiyo kukatokea timbwili hilo kwani mlinzi wa pale alikuwa anamsaidia yule dada aliyeniibia.”
“Wakati nikiwa najihami maana yule mlinzi alikuwa akinikaba, nilimpiga kibao, akakimbilia bunduki yake na kuanza kuikoki akitaka kunipiga risasi.
“Baada ya kuona amefikia hatua hiyo niliingia haraka kwenye gari langu na kuondoka zangu kwani nilihisi walikuwa na njama moja ya kuniibia mafuta na walipoona nimerudi kulalamika ndiyo wakaamua kunifanyia vurugu, kweli sikufurahishwa na tabia yao kwanza ni wezi wakubwa wa mafuta hao,” alisema Wolper.
Chanzo:GPL
NUNUA FILAMU KUTOKA STEPS ENTERTAINMENT: TUNAKUFIKISHIA POPOTE PALE ULIPO:
Piga namba hizi: 0673 348 364 au 0754 256 489.
KAMA UNATAKA KUWA WAKALA WA KUSAMBAZA FILAMU POPOTE PALE:
Piga namba hizi: 0673 348 364 au 0754 256 489.
Filamu Zilizotoka Hivi Sasa >>>>HIZI HAPA
Comments
comments